Mende huchukiwa sana na watu na huhusishwa na uchafu na maradhi. Lakini wajua kwamba wadudu hawa wana manufaa makubwa sana kwa binadamu?
Mjini Havana, nchini Cuba kuna aina ya mende ambao hufugwa kama wanyama vipenzi na hata visa vyao husimuliwa kwenye hadithi, anasimulia Mary Colwell.
Kwenye kisa kimoja, mende kwa jina Martina huwafanyisha mtihani wanaotaka kumchumbia kwa kuwaudhi kila wanapomtembelea.
"Mwaga kahawa kwenye viatu vyao uone watalichukulia vipi hilo,” anapendekeza nyanyake Martina. "Ni muhimu sana kujua mumeo mtarajiwa hufanya nini anapokasirika – mtihani wa kahawa hufanikiwa.”
Kuna aina 4,500 ya mende, na ni aina nne pekee ambao huwa waharibifu.
Wengi hawaishi karibu na nyumba za watu na hutekeleza jukumu muhimu katika ikolojia kwa kula vitu vilivyokufa na vinavyooza.
Baadhi wana sifa nzuri na huishi pamoja na kusaidiana katika kutafuta chakula na makazi. Wana uwezo wa kuishi katika mazingira magumu. Aina moja kwa jina Eublaberus posticus wanaweza kuishi mwaka mmoja kwa kunywa maji pekee.
Wale wazito zaidi, huwa na uzani wa gramu 35, na urefu wa sentimeta 8 na huishi Australia. Wale wadogo zaidi huishi Ulaya na Amerika Kaskazini na wana urefu wa sentimeta moja pekee.
Badala ya kuwachukia, wanasayansi huwafurahia sana na kuwatumia kwa manufaa ya binadamu. Mwaka 1999, mende walitumiwa na Prof Robert Full katika Chuo Kikuu cha California, Berkley, kumpa wazo la kuunda roboti ya miguu sita iliyosonga upesi na kwa urahisi.
Mende huwa thabiti sana, na wakianguka huwa wanainuka upesi na kwa urahisi kwa kutumia mabawa.
Miguu ya mende pia imekuwa ikitumiwa na wavumbuzi wanaotengeneza miguu bandia ya kutumiwa na binadamu.
Kuna pia mende ambao wamekuwa wakiunganishwa na kompyuta ndogo inayowekwa mgongoni na kuongozwa kufika maeneo ambayo mwanadamu hawezi kufika.
Comments
Post a Comment