Hadithi Lucas 14

Sehemu ya - 14

Baada ya maaskari hao 3 waliobaki kumuhoji Stella kumwambia Stella kuwa ingawa awali alisema kuwa hamjui Nancy mke wa Lucas kwa kumuona kwa macho bali anamjua kwa kumuona tu kwenye picha, tena baada ya yeye Stella kuanza kuishi na Lucas, sasa awaeleze ukweli je na Nancy naye pia yupo kwenye hilo grupu lao?, Stella aliwaangalia maaskari wale kwa uso na macho ya huruma kuashiria kuwa alikuwa ameshakata tamaa kabisa ya maisha yake na pia alikuwa ameshachoka na maswali yao lakini alikuwa hana jinsi hivyo ilibidi tu awajibu swali lao hilo walilokuwa wamemuuliza kuhusu Nancy mke wa Lucas.

Stella huku akiwa na huzuni na hali iliyoashiria kuwa ameshakata kabisa tamaa ya kuishi na kuwa huru tena, aliwajibu maaskari wale na kuwaambia kuwa kusema ukweli kama alivyokuwa amewaambia mwanzo kuwa yeye hamfahamu Nancy kabisa na wala hajawahi kumuona kwa macho ila alimuona tu kwenye picha zilizokuwa nyumbani kwa Lucas ingawa sasa Lucas ameshazitoa picha zake hizo ukutani na sehemu nyingine alikokuwa ameziweka.

Baada ya Stella kuwajibu hivyo maaskari hao, maaskari hao walimuuliza tena Stella na kumwambia kuwa kwahiyo Nancy hajui chochote kabisa kuhusu mtu yule aliyewavamia yeye na Lucas? Na pia hajui kabisa kuhusu biashara hizo haramu za Thomas? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa ndio Nancy hajui chochote kuhusu yule mtu aliyewavamia na pia hajui chochote kuhusu biashara anazozifanya shemeji yake Thomas, yani yeye ni victim tu, lakini hahusiki na chochote na wala hajui chochote kuhusu grupu lao hilo.

Baada ya Stella kuwajibu hivyo maaskari hao alijua kuwa amemaliza kuwajibu maaskari hao na labda watamuachia sasa apumzike kwani alikuwa amechoka sana na alikuwa na maumivu karibia sehemu za mwili wake wote, na pia isitoshe maaskari hao wamekuwa wakimuhoji siku nzima mpaka muda huo tayari ilikuwa ni usiku wa saa nne bado tu walikuwa wakiendelea kumuhoji. Wakati Stella akiwaza hivyo mara alishtuliwa tena na maaskari hao waliomuuliza tena swali jingine kuwa na Mary je mke wa Thomas naye anahusika na anajua chochote kuhusu huo uhalifu na hizo biashara anazozifanya mume wake Thomas? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa hata Mary mke wa Thomas naye hajui chochote na itakuwa tu anajua mume wake ni mtu mwema sana.

Baada ya jibu hilo la Stella, maaskari hao walimuuliza tena Stella swali jingine kuwa je na Lucas naye anafahamu hizo biashara za kaka yake? Je naye wako naye pamoja?

Baada ya maaskari waliokuwa wakimuhoji Stella kumuuliza Stella kuwa je na Lucas naye anafahamu hizo biashara za kaka yake? na je naye pia wako naye pamoja kwenye hilo grupu lao? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa Lucas hajui chochote kuhusu biashara za kaka yake na mambo mengine ya uhalifu anayoyafanya kaka yake huyo na isitoshe Lucas anamuamini sana kaka yake huyo.

Baada ya jibu hilo la Stella, maaskari wale walimwambia Stella kuwa kama Lucas hajui chochote kuhusu biashara hizo za kaka yake je ni sababu ipi hasa iliyopelekea kaka yake huyo kutaka kumuua?

Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa yeye hajui kwa undani zaidi ingawa mara kwa mara kaka yake huyo alikuwa akiwaambia kuwa anataka kumuua mdogo wake huyo kwasababu kwasasa kampuni na biashara za mdogo wake huyo zinafanya vizuri sana, hivyo kama akimuua mdogo wake huyo itakuwa rahisi kwake kuitumia kampuni hiyo ya mdogo wake kwa ajili ya biashara zake hizo za madawa ya kulevya na kufanya uhalifu wake mwingine bila ya kushtukiwa kwa urahisi kwasababu kampuni hiyo ya Lucas ni moja kati ya makampuni yanayoheshimika na kuaminika hapa nchini.

Baada ya jibu hilo la Stella, maaskari hao walimuuliza tena Stella na kumwambia kuwa sasa kama wangefanikiwa kumuua Lucas mbona ni hali iliyowazi kabisa kuwa hiyo kampuni, biashara na mali nyingine za Lucas zingerithiwa na mke wake Nancy pamoja na mtoto wake Henry, sasa mbona huyo Thomas angekuwa amefanya kazi ya bure ya kumuua mdogo wake huyo wakati hizo mali anazozitaka zingekuwa mikononi mwa watu wengine na sio yeye Thomas?

Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa Thomas alipanga kuwa akishafanikiwa kumuua Lucas angekuja kumuua na Nancy mke wake Lucas pia, tena kumuua Nancy alikuwa akisema kuwa ingekuwa ni rahisi zaidi kwani yeye ni mwanamke hivyo isingekuwa shida sana kummaliza, na mtoto wao Henry kwasababu ni mdogo alisema angekuwa anammaliza kidogo kidogo kwa madawa ya kulevya na mpaka angekuwa mkubwa angekuwa ni teja hivyo hata asingekuwa na uwezo tena wa kufatilia hizo mali za baba yake. Baaada ya jibu hilo la Stella maaskari wale walishusha pumzi kwa nguvu na kukawa kimya kwa dakika kadhaa kuonyesha kila mmoja alikuwa akiwaza la kwake kichwani mwake.

Maaskari hao waliendelea kumwambia Stella kuwa sasa awaeleze ilikuaje kuaje mpaka yule mtu akawavamia Lucas na mke wake Nancy kama Nancy hahusiki na hajui chochote kuhusu hilo? na pia ilikuwaje huyo mtu akajua kuwa Lucas siku hiyo atakwenda kumchukua mke wake Nancy kazini kwake ndio maana na yeye akaenda huko kazini kwa Nancy ili kumsubiria Lucas?

Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa Thomas kaka yake Lucas ni muuza madawa na pia ni muhalifu aliyekubuhu hivyo pale kazini kwa Lucas amempandikiza mtu ambaye ndio huwa anampa information zote jinsi mambo yanavyokwenda pale kazini kwa Lucas, yani huyo mtu anamwambia kila kitu kama vile nani kaingia na nani ametoka.

Baada ya Stella kusema hivyo maaskari hao walishusha tena pumzi kwa nguvu na waliona hapo kuna maswali mengi sana ambayo yanahitaji ufafanuzi na itabidi wamuulize maswali yote hayo Stella kabla hawajamwachia Stella kwenda mahabusu na wao kurudi majumbani kwao kupumzika na pia ikibidi itabidi wamuulize hata kama itafika asubuhi.

Hivyo maaskari hao walimuuliza Stella kuwa je huyo mtu aliyepandikizwa kazini kwa Lucas ni nani? Stella akajibu kuwa huyo mtu ni mlinzi wa kwenye ofisi za Lucas. Maaskari wale waliendelea kumuuliza tena Stella kuwa je hapo kazini kwa Lucas kuna walinzi wangapi? Stella aliwajibu na kuwaambia kuwa wapo walinzi wanne na mara nyingi asubuhi wanalinda wawili na usiku wanalinda wawili, na wenyewe walinzi hao ndio wanajua jinsi ya kupeana zamu ya kulinda mchana na usiku hivyo kati ya hao wanne mmoja ni kijana wa Thomas.

Baada ya Stella kusema hivyo, maaskari hao walimuuliza tena Stella kuwa je sasa siku hiyo Lucas na mke wake Nancy waliyovamiwa Thomas alijuaje kuwa Lucas anakwenda kazini kwa mke wake siku hiyo kumchukua?

Stella aliwajibu maaskari upelelezi wale na kuwaambia kuwa mlinzi ambaye alikuwa amepandikizwa na Thomas ili kufatilia nyendo za Lucas na mambo yote yanayoendelea pale kazini kwa Lucas ndio alimpigia simu Thomas na kumwambia kuwa Lucas muda huo anakwenda kazini kwa mke wake Nancy kumchukua na hivyo Thomas ndio akamtuma yule mtu yaani Devi kwenda kazini kwa Nancy ili akafanye kila analoweza ikiwezekana wampe lifti ili atimize adhma yake hiyo kwani Thomas alikuwa ameshajaribu kila njia ili kumuua Lucas lakini ilishindikana hivyo siku hiyo ndio aliona ni nafasi nzuri sana kutimiza malengo yake hayo.

Pia Stella aliwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa ila yeye hafahamu ilikuaje mpaka Lucas akamwambia huyo mlinzi kuwa anakwenda huko kazini kwa mke wake Nancy ila anachofahamu ni kuwa huyo mlinzi ndio aliyempigia simu bosi wao Thomas na Thomas naye ndio akamtuma Devi aende kazini kwa Nancy kabla Lucas hajafika.

Baada ya jibu hilo la Stella maaskari hao walimwambia Stella kuwa sasa ilikuaje huyo Devi aliyetumwa na Thomas akawahi kufika kazini kwa Nancy kabla ya Lucas wakati Thomas aliambiwa kuwa Lucas anakwenda kumchukua mke wake Nancy wakati Lucas ameshaondoka?

Stella aliwajibu maaskari hao wa upelelezi na kuwaambia kuwa Devi alitumia usafiri wa pikipiki ambazo siku hizi zinajulikana zaidi kama bodaboda hivyo ilikuwa rahisi kwake kukwepa foleni na hivyo kuwahi kufika kazini kwa Nancy kabla Lucas hajafika sehemu hiyo. Baada ya jibu hilo la Stella ndio maaskari wa upelelezi Gabriel na Saidi wakakumbuka jinsi mashuhuda wa ajali ya Lucas na mke wake Nancy walivyowaambia polisi waliofika kwenye eneo la tukio kuwa walishangaa kuona mtu mmoja kati ya watu waliokuwa kwenye hilo gari la kina Lucas mara tu baada ya kupata ajali yeye alitoka haraka haraka na akapanda kwenye pikipiki iliyofika mahali hapo muda mfupi baada ya kina Lucas kupata ajali, na mtu huyo baada ya kupanda kwenye pikipiki hiyo, pikipiki hiyo iliondoka kwa kasi sana. Hivyo baada ya kukumbuka hilo, askari wa upelelezi Saidi akamuuliza Stella kuwa je ile pikipiki aliyoipanda huyo Devi mara tu baada ya kupata ajali na kina Lucas na yeye kufanikiwa kutoka wa kwanza ndio hiyo anayoiongelea? Stella alijibu ndio. Baada ya jibu hilo la Stella maaskari hao wa upelelezi walimuuliza Stella kuwa kwahiyo hiyo pikipiki ilikuwa ikiwafatilia kina Lucas? Stella akajibu ndio, pikipiki hiyo ilikuwa ikiwafatilia kina Lucas toka walipotoka ofisini kwa Nancy ili kukitokea mtafaruku wowote yule aliyekuwa anaendesha pikipiki naye aweze kusaidia.

Stella aliendelea kuwaambia maaskari wale wa upelelezi kuwa Thomas alimtuma Devi na kijana mwingine ambaye ndio alikuwa akiendesha pikipiki hiyo ili waende kazini kwa Nancy na walivyofika kazini kwa Nancy, Devi yaani yule mtu aliyewaomba lifti kina Lucas na Nancy alishuka na mwenzake alibaki kwenye pikipiki eneo ambalo alikuwa akiona kila kitu kinachoendelea, na hata Lucas alivyofika na kumchukua mke wake Nancy na pia kumpa lifti Devi na kuanza kuondoka mwenzake huyo aliyebaki kwenye pikipiki alianza kuwafatilia ili kuhakikisha usalama wa Devi.

Kwa majibu hayo ya Stella maaskari hao waliokuwa wakimuhoji walianza kuona kuwa maswali yao mengi ambayo yalikuwa na viulizo kwa muda mrefu yalikuwa yanaanza kujibiwa na hivyo hawakuchoka na waliendelea kumuuliza maswali Stella.

Ingawa maswali yao mengi waliyokuwa nayo yalikuwa kwa kiasi fulani yameshajibiwa na Stella lakini bado maaskari hao walikuwa wakijiuliza je mlinzi huyo aliyepandikizwa ofisini kwa Lucas atakuwa alitumia njia gani kujua kama Lucas alikuwa anakwenda kumchukua mke wake Nancy kazini kwake mpaka naye akamwambia Thomas? Maaskari wale walikosa jibu na hivyo walibaki kusema hilo swali atalijibu yeye mwenyewe Lucas na huyo mlinzi aliyepandikizwa na Thomas.

Pia maaskari hao walimuuliza Stella kuwa amesema kuwa huyo mlinzi aliyepandikizwa na Thomas ndio alimpigia simu Thomas na kumwambia kuwa Lucas muda huo anaondoka na kwenda kazini kwa mke wake lakini mbona wao kama maaskari walivyochukua simu za wafanyakazi wote na kuzichunguza na pia walivyozichunguza namba zao huko kwenye makampuni ya simu wala hawakuona mawasiliano ya mfanyakazi yeyote wa Lucas kwenda kwa Thomas au kwa mtu yeyote ambayo yangewapa mwanga wa tukio lile la kuvamiwa Lucas akiwa na mke wake Nancy? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa Thomas ana mtandao wa vijana ambao ni hatari sana na ambao wako makini sana na wanachokifanya yani uhalifu wao ni wa kiwango cha juu, hivyo hata mawasiliano yao ya kihalifu hata siku moja huwa hawatumii simu au line za simu zao za siku zote zinazojulikana na watu, na pia karibia kila baada ya muda mfupi huwa wanabadilisha line hizo za simu na kununua nyingine.- Baada ya jibu hilo la Stella maaskari wale walimwambia Stella kuwa amesema kuwa Thomas ana mtandao wa vijana ambao ni hatari sana na ambao wako makini sana na wanachokifanya hivyo ina maana hata yeye pia ni hatari sana na yuko makini sana na anachokifanya kwenye mambo yao hayo ya uhalifu? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa ndio na yeye pia yuko hivyo. Baada ya jibu hilo la Stella maaskari wale walitabasamu na walimwambia Stella kuwa kama na yeye yuko makini mbona ameshindwa kutimiza kusudio la huyo bosi wao Thomas kumuua Lucas na mpaka sasa yupo mikononi mwao? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa hiyo ni ajali tu kazini na mtu yeyote inaweza kumtokea.

Baada ya jibu hilo la Stella mmoja wa maaskari wale alimpiga kibao Stella na kumwambia kuwa anaanza kuleta ujeuri wake tena!? Hivyo ajibu maswali yao kwa adabu asifikiri yupo na wauza unga wenzie hapo.

Wakati Stella akiendelea kusikilizia maumivu ya kibao alichokuwa amepigwa na mmoja wa maaskari hao, maaskari hao waliendelea kumuuliza Stella maswali na mwishowe walimuuliza je baada ya huyo mtu kushindwa kumuua Lucas kilitokea nini? Stella aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa baada ya huyo mtu yaani Devi kushindwa kumuua Lucas alivyofika kwa Thomas, Thomas bado nusu amuue yeye sema wao walimuwahi na kumzuia bosi wao huyo asifanye hivyo kwani Devi ni mmoja wa vijana wachache wa muhimu sana kwenye kundi lao na mara nyingi kazi ngumu ndio huwa anatumwa yeye na huwa hashindwi na hata wao siku hiyo walishangaa sana alivyoshindwa.

Stella aliendelea kuwaambia maaskari hao kuwa, baada ya kutulia na hasira kumuisha, Thomas aliendelea kumlaumu Devi kuwa sasa kwanini hakumpiga Lucas risasi ya kichwa na badala yake akampiga ya begani kwahiyo alitegemea akimpiga huko begani ndio atakufa? Maaskari walimuuliza Stella kuwa je baada ya Thomas kumlaumu na kumwambia hivyo huyo Devi kuwa kwanini hakumpiga Lucas risasi ya kichwani, je huyo Devi alijibu nini?-

Stella aliwaambia maaskari hao kuwa huyo Devi alijibu kuwa alipitiwa tu kwasababu hakutegemea kabisa kama Lucas atafungua kioo na kuanza kupiga kelele. Pia kama angempiga Lucas risasi ya kichwani hata yeye Devi angeweza kufa pia kwani wangeweza kupata ajali mbaya zaidi ya ile waliyoipata. Na baada ya mtu huyo kusema hivyo Thomas alisema kuwa kwani angekufa yeye kungekuwa na hasara gani?

Stella aliendelea kuwaambia maaskari hao kuwa na baadaye iliamriwa kuwa yule mtu aliyekuwa akiitwa David Kituka na ambaye alikuwa akijulikana kama Devi aondoke aende nje ya nchi kwanza mpaka patulie ndio arudi. Baada ya jibu hilo la Stella, maaskari wale walimuuliza tena Stella kuwa je mtu huyo alikimbilia nchi gani? Stella aliwajibu na kuwaambia kuwa alikimbilia Philippines kwani huko nako kuna mtu wao anayehusika na biashara zao.

Baada ya jibu hilo la Stella, maaskari hao waliona kuwa sasa wanaweza kurudi majumbani kwao kupumzika kwani walikuwa wameshapata information za muhimu sana kutoka kwa Stella kuhusu kesi ya kina Lucas na pia waliamua huyo Stella apelekwe mahabusu mpaka watakapoamua kuendelea kumuhoji tena na hatua zaidi zitakapochukuliwa dhidi yake na hao wenzake wakiongozwa na Thomas kaka yake Lucas.

Maaskari hao walirudi makwao saa kumi ya alfajiri. Walivyofika makwao askari Saidi alimkuta mke wake akiwa bado yupo macho na alivyomuuliza kuwa kwanini hajalala mpaka muda huo? Mke wake huyo alimjibu na kumwambia kuwa anafikiri atalala wakati yeye hajarudi na alivyojaribu kumpigia simu ilikuwa haipatikani!? Askari wa upelelezi Saidi alimjibu mke wake huyo na kumwambia kuwa anafahamu kazi zake jinsi zilivyo, na pia siku hiyo sio mara ya kwanza yeye kuchelewa kurudi nyumbani na simu zake kuwa hazipatikani, kwani imekuwa ikimtokea mara kwa mara sasa kwanini ameamua kujitesa hivyo kwa kutokulala mpaka alfajiri hiyo wakati anafahamu kabisa kazi zake zilivyo. Baada ya jibu hilo la askari Saidi kwa mke wake, mke wake huyo alimwambia askari huyo wa upelelezi Saidi kuwa, hata kama yeye Saidi ni askari lakini yeye sio askari hivyo ikitokea yeye kuchelewa na simu zake kutopatikana huwa anashikwa na wasiwasi kidogo kwa kudhani kuwa labda amepatwa na mabaya lakini sasa atalala maana roho yake tayari ina amani baada ya kumuona amerudi nyumbani akiwa salama na mzima wa afya. Baada ya mke wa askari wa upelelelezi Saidi kumwambia hivyo mume wake huyo, alipanda kitandani na kulala na alipitiwa na usingizi baada ya muda mfupi tu tangu apande kitandani.

Baada ya kama nusu saa hivi kupita tangu mke wa askari wa upelelezi Saidi kupanda kitandani na kulala alishtuka tena na kwa mshangao wake alimkuta mume wake huyo akiwa bado yupo macho na amekaa vilevile kitandani huku akiwa ameshika tama na hivyo alimuuliza mume wake huyo kwa upole kuwa je kwani ana tatizo gani!? Mbona anaonekana ni mtu mwenye mawazo mengi sana na pia hana raha kabisa tangu arudi!? kwani siku zingine hata akichelewa kurudi nyumbani kutoka kwenye hizo kazi zake huwa anafikia kulala na ana aamka akiwa mwenye furaha na tabasamu pana usoni mwake, kwani leo amepatwa na nini hasa mpaka kuwa kwenye hali hiyo!?

Na baada ya kusema maneno hayo, mke huyo wa askari wa upelelezi Saidi alimwambia mume wake huyo kuwa anaomba asimfiche kwani yeye ni mke wake labda akimueleza kinachomsibu anaweza kujua cha kumshauri.

Baada ya mke wake huyo kusema hivyo, askari upelelezi Saidi alimgeukia mke wake huyo na kumwambia kuwa ingawa yeye ni askari na watu wakati wote wanajua kuwa wao maaskari wana roho ngumu sana na pia hawajali na kuna wengine huwa wanafikia mpaka kuwa na shaka kama wanamuabudu Mungu lakini ukweli ni kuwa wao ni binadamu pia kama walivyo wanadamu wengine na kuna wakati roho ya ubinadamu inawaingia. Na sababu hasa inayomfanya yeye awe kwenye hali hiyo aliyokuwa nayo ni kuwa leo amegundua kuwa ameinyanyasa na kuisulubisha roho ya mtu ambaye hana hatia kabisa na wala hajui Mungu atamlipa nini kwa hili. Mke wake alishangaa sana kusikia hilo kutoka kwa mume wake huyo ambaye siku zote amekuwa akiamini ni mtu jasiri na asiyekuwa na chembe ya uoga hata kidogo, hivyo alitaka kujua zaidi na hivyo alimuuliza mume wake huyo kuwa je ni nani huyo na kwanini amfanyie hivyo!?

Askari upelelezi Saidi alimjibu mke wake huyo na kumwambia kuwa kwasababu za kiusalama za kazi yake hawezi kumwambia chochote zaidi ila atamwambia tu kijuu juu kuwa leo ndio amegundua kuwa walimpa mtu kesi ya kutaka kuua wakati hahusiki kabisa na wameshamtesa sana na usiku huu anavyoongea huyo mtu bado yuko mahabusu.

Baada ya askari upelelezi Saidi kumwambia hivyo mke wake, mke wake huyo akamwambia kuwa sasa si wamuachie huru huyo mtu kama wamegundua kuwa hana kosa lolote, na pia wao walikuwa wapo kazini hivyo asijilaumu sana na kujiona ni mwenye makosa, na kama huyo mtu alikuwa hana makosa ndio maana Mungu amemuona na ndio maana leo wamejua. Na kwasababu hataki kumwambia chochote kwa undani zaidi basi sasa alale na apumzike na asisononeke sana kwani yeye alikuwa akifanya kazi yake na hakukusudia kumuonea au kumuumiza mtu yeyote. Baada ya maneno hayo ya mke wake, askari upelelezi Saidi alipata amani kidogo na hivyo akapanda kitandani kulala na muda mfupi akapitiwa na usingizi. Akiwa usingizini, askari upelelezi Saidi aliota Nancy mke wa Lucas akiwa mbele yake huku akiwa amefungwa mikono yake kwa pingu na alikuwa akilia sana huku akimuangalia yeye kwa huzuni.

Nyumbani kwa Lucas nako ule usiku Lucas alikuwa amekaa sebuleni akiangalia TV huku akiwa amejipumzisha na kutafakari yaliyompata. Lucas alikuwa akiwaza kuwa je kama asingeamua kuangalia mpira na hivyo kula chakula mara tu kilivyotengwa je sasa hivi angekuwa ameshakufa? -na kama angekuwa amekufa je angekuwa wapi kwasasa! Na je kama yeye angekufa, mtoto wake Henry ingekuaje!? Pia Lucas aliendelea kumshukuru rafiki yake mzungu aliyempa zile peni za camera alivyokwenda Marekani maana bila hivyo mtoto wa watu Fatuma angeozea jela maskini kwa kosa ambalo wala hakulitenda yeye kabisa.

Wakati Lucas akiendelea kuwaza yote hayo mara simu yake ya mkononi iliita na alivyopokea alikuwa ni Mary mke wake Thomas ambaye alikuwa akiongea huku analia. Lucas alishtuka kidogo na hivyo haraka haraka alijua kutakuwa na tatizo kubwa huko nyumbani kwa kaka yake Thomas na inawezekana mtoto wake Henry amepatwa na tatizo kubwa au ni kaka yake Thomas ndio atakayekuwa amepatwa na tatizo, hivyo alimwambia Mary mke wa Thomas kuwa hebu anyamaze kwanza na amweleze vizuri kimetokea nini huko kwao? Mbona analia? Mary huku akijitahidi kunyamaza alianza kumwambia Lucas kuwa kuna matatizo makubwa yametokea hapo nyumbani kwao na akanyamaza. Lucas alishtuka sana kusikia hivyo, na akamuuliza Mary kuwa je ni matatizo gani hayo yaliyotokea? Hebu amueleze ni nini kimetokea? Mary akamwambia Lucas kuwa limekuja kundi la maaskari kama sita hivi na kumchukua mume wake Thomas. Yani wamemkamata kama jambazi vile. Baada ya Mary kusema hivyo, Lucas akamuuliza shemeji yake huyo kuwa je sababu hasa iliyofanya kumkamata kaka yake huyo tena kama jambazi ni nini? Mary mke wa Thomas akamjibu Lucas na kumwambia kuwa hata yeye hafahamu na alivyojaribu kuwauliza wakamjibu kuwa asiwapotezee muda kama anataka kufahamu aende kesho kituoni atajua. Basi baada ya maelezo hayo ya Mary, Lucas akamwambia Mary kuwa inawezekana kuna watu wanawachezea michezo mibaya yeye na kaka yake huyo hivyo ukute baada ya kuona wameshindwa kumuua yeye Lucas, sasa wanaanza kuwachafua kwa kuwasingizia mambo yasiyofaa ngoja wataenda kujua huko kituoni hiyo kesho ili kujua sababu hasa iliyofanya maaskari hao kumkamata kaka yake Thomas tena kama jambazi!

Lucas pia aliendelea kumwambia Mary mke wa Thomas kuwa kwasababu tayari ilikuwa ni usiku wa saa nne hivyo hawawezi kufanya chochote kwa muda huo na inabidi ajikaze tu mpaka asubuhi na yeye Lucas atakwenda hapo nyumbani kwao asubuhi na mapema ili waone nini cha kufanya.

Baada ya kumaliza kuongea na Mary mke wa Thomas, Lucas alikuwa kama amechanganyikiwa na alibaki kusema sijui ni nani huyo anayeichezea familia yao! Maana mwanzo walikuwa wakimuandama yeye na sasa inaonyesha wameanza kumuandama pia na kaka yake Thomas.

Mpaka wakati ambao Thomas alikuwa anakamatwa, Thomas alikuwa hajajua kama Stella naye alikuwa amekamatwa kwani Lucas alikuwa hajamwambia kaka yake Thomas wala ndugu au rafiki- yake yeyote kuhusu kukamatwa kwa Stella, na sababu kubwa hasa iliyofanya asifanye hivyo ni kwasababu alikuwa akiona aibu kuwaeleza ndugu zake hao kuwa hata huyo mwanamke wa pili aliyekuwa anaishi naye na aliyekuwa na malengo ya kumuoa hapo baadaye baada ya kumuacha mke wake Nancy kwa talaka naye alitaka kumuua tena kwa kumuwekea sumu kwenye chakula! kwani kwa kiasi fulani Lucas aliona kuwa labda ndugu zake hao wangemuona mpumbavu kwa kuamua kuishi na mwanamke mwingine mwaka mmoja na miezi kadhaa tu tangu mke wake Nancy akamatwe, hivyo ndio maana aliamua kunyamaza kwanza na alipanga kuwa huko baadaye ndio aje tu kuwaambia kijuujuu kuwa alimuachaga huyo Stella.
SEHEMU YA KUMI NA TANO 15

Comments