Hadithi lucas 2

Sehemu ya - 2

Baada ya maaskari upelelezi Saidi na Gabriel kukabidhiwa faili la mfanyabiashara Lucas na bosi wao Jamal na wao kuliangalia kwa haraka haraka, maaskari hao wa upelelezi walisimama na kupiga saluti na kuondoka ofisini humo kwa bosi wao ili kwenda kuanza kazi ya kupeleleza swala hilo.

Maaskari upelelezi Saidi na Gabriel waliamua kwanza kufanya kikao cha haraka haraka kati yao wawili ili kuona mwanga wa pa kuanzia na mwisho walikubaliana kuwa waende hospitali alikokuwa amelazwa Lucas ili wakaongee nae kama ana nguvu ila kama hana nguvu basi waongee na mke wake kwani kuna maswali mengi wanaona ambayo yalikuwa yakihitaji majibu kutoka kwa Lucas mwenyewe pamoja na mke wake Nancy. Hivyo baada ya kikao chao hicho kilichochukua kama dakika 20 hivi, maaskari upelelezi hao waliamua kwenda hospitali alikokuwa amelazwa Lucas akiugulia kidonda chake kilichotokana na risasi aliyopigwa na huyo mtu waliyempa lift.

Baada ya kikao chao cha haraka haraka ambacho kilichukua muda wa kama dakika ishirini hivi, maaskari upelelezi Saidi na Gabriel waliondoka na kuanza safari ya kuelekea hospitali alikokuwa amelazwa Lucas. Walivyofika kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Lucas, walikuta mfanyabiashara huyo akiwa hayupo na walipojitambulisha kuwa wao ni kina nani na wanamuulizia mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa amelazwa mahali hapo, manesi waliwajibu kuwa Lucas amesharuhusiwa siku hiyo kurudi nyumbani kwake baada ya afya yake kuimarika. Baada ya majibu hayo ya manesi, maaskari hao wa upelelezi waliondoka wodini hapo na kwenda kwenye gari lao ambalo walikuwa wamekwenda nalo na walivyoingia tu kwenye gari lao hilo walianza kushauriana nini cha kufanya baada ya kukuta Lucas akiwa ameshatolewa hospitalini hapo alipokuwa amelazwa hivyo baada ya majadiliano ya kama dakika 3 hivi walikubaliana kuwa basi waende huko huko nyumbani kwa Lucas na wakifika huko waanze kumuhoji Lucas na ndio wamalizie kumuhoji mke wa Lucas yaani Nancy.

Baada ya maaskari upelelezi Saidi na Gabriel kufika nyumbani kwa Lucas walijitambulisha getini kwa mlinzi kuwa wao ni kina nani na mlinzi alivyoridhika baada ya kuona vitambulisho vyao aliwaruhusu waingie ndani. Walivyofika ndani walimkuta Lucas akiwa ana nguvu na pia akiwa amechangamka kidogo na alikuwa akinywa supu muda huo hapo sebuleni huku akiangalia TV pamoja na mke wake Nancy na mtoto wao Henry ambaye alikuwa na miaka 2 tu.

Walivyokaribishwa ndani maaskari upelelezi hao Gabriel na Saidi walijitambulisha kwa Lucas na mke wake na kuwaeleza kuwa wao ni maofisa wa upelelezi na wamekwenda hapo kwa ajili ya uchunguzi wa kesi yao ya kuvamiwa na mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi ambaye pia alikuwa amewaomba lifti.

Pia maaskari hao wa upelelezi waliendelea kumwambia Lucas kuwa kwa hali waliyomkuta nayo wana uhakika kabisa ataweza kuwapa ushirikiano wa kutosha na hivyo kuwaeleza kila kitu kilichotokea siku hiyo. Hivyo Maaskari hao wa upelelezi walimuomba Nancy mke wa Lucas awape nafasi kidogo ili waweze kuongea na mume wake huyo. Baada ya kuambiwa hivyo na maaskari hao wa upelelezi Nancy mke wa Lucas aliondoka sebuleni hapo alipokuwa amekaa na mume wake na kwenda jikoni ili kuwasaidia wasichana wao wa kazi waliokuwa huko jikoni wakipika.

Baada ya Nancy kuondoka na kwenda jikoni, Gabriel na mwenzake Saidi walianza kumuuliza maswali Lucas huku wakipokezana na hivyo walianza kumuuliza Lucas kuwa je anakumbuka siku hiyo aliyovamiwa na huyo mtu kilitokea nini mpaka kupelekea huyo mtu kuwa kwenye gari lao na kumpiga yeye risasi kwenye bega lake la kulia na mwishowe wakapata ajali na huyo mtu kukimbia?

Lucas alikaa kimya kidogo na kufikiri kwa dakika kadhaa, na baada ya dakika kadhaa kupita, Lucas aliwaeleza maaskari hao wa upelelezi kuwa anachokumbuka siku hiyo ni kuwa mke wake Nancy alimpigia simu na kumwambia kuwa gari lake ni bovu hivyo alimuita fundi kulitengeneza lakini fundi huyo amemueleza kuwa ubovu ni mkubwa kidogo na uwezekano wa kupona siku hiyo ni mdogo sana na amelichukua gari hilo na kwenda nalo gereji hivyo anaomba aende akamchukue huko kazini kwake ili warudi wote nyumbani na walikubaliana aende kumpitia kwenye mida ya saa kumi na moja jioni.-

Wakati Lucas akiwaeleza hivyo maaskari hao wa upelelezi, maaskari hao walikuwa wakimsikiliza na kuandika baadhi ya vitu kwenye madaftari yao madogo waliyokuwa wamekwenda nayo na pia walikuwa wakimrekodi Lucas kila alichokuwa akiwaambia.-

Baada ya Lucas kumaliza kuwaelezea jinsi mke wake Nancy alivyompigia simu na kumuomba aende akamchukue kazini kwake kwasababu gari lake lilikuwa bovu na hivyo walikubaliana kuwa Lucas aende kumchukua kazini kwake huko saa kumi na moja jioni maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je ni nini kilitokea baada ya kumaliza kuongea na mke wake huyo kwenye simu na kukubaliana naye kuwa aende kumchukua hiyo saa kumi na moja ya jioni?-

Lucas aliwajibu maaskari hao kuwa hamna cha zaidi kilichoendelea sana sana yeye aliendelea tu na kazi zake mpaka ilivyofika mida ya saa kumi jioni yeye ndio akaondoka kazini kwake na kwenda kumpitia mke wake huko kazini kwake.-

Maaskari hao wa upelelezi walimuuliza Lucas kuwa je wakati anaongea na mke wake Nancy kwenye simu yeye Lucas alikuwa wapi? Alikuwa ofisini kwake au nje ya ofisi au mahali gani? Lucas aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa wakati alivyokuwa akiongea na mke wake Nancy kwenye simu yeye alikuwa tu ofisini kwake. Baada ya Lucas kujibu swali hilo, maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je alikuwa na nani ofisini humo wakati akiongea na mke wake kwenye simu? Lucas aliwajibu maaskari hao na kuwaeleza kuwa alikuwa tu peke yake wala hakukuwa na mtu yeyote. Na pia maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je mke wake huyo alimpigia simu kwa kutumia simu yake ya mezani au ya mkononi? Lucas aliwajibu maaskari hao kuwa alitumia simu yake ya mkononi maana mara nyingi sana mke wake huyo huwa anampigia simu kupitia simu yake ya mkononi na mara chache sana ndio huwa anatumia simu yake ya mezani.

Baada ya Lucas kuwaeleza hivyo maaskari hao wa upelelezi, maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je hakumbuki kabisa kama labda kulikuwa na chombo chochote cha usafiri kama pikipiki au gari ambacho kilikuwa kikimfatilia kutoka huko kazini kwake alikotoka mpaka huko kazini kwa mke wake alikokuwa amekwenda? Lucas aliwajibu maaskari hao kuwa hakumbuki kabisa kama kulikuwa na gari au pikipiki au chombo cha aina yoyote ya usafiri kikimfatilia wakati alipotoka kazini kwake kwenda ofisini kwa mke wake.

Baada ya Lucas kujibu hivyo maaskari hao waliandika mambo kadhaa kwenye madaftari yao na waliendelea kumuuliza Lucas maswali ambapo walimuuliza kuwa je baada ya kufika ofisini kwa mke wake ilikuwaje? Lucas aliwajibu wapelelezi hao kuwa alivyofika hapo ofisini kwa mke wake alimkuta mke wake akiwa nje ya ofisi zao akimsubiri na mke wake huyo alivyofungua mlango wa mbele wa gari yao kabla hajapanda kwenye gari alimwambia kuwa kuna mtu hapo anaomba lifti kwani anasema kuwa eti anakwenda maeneo wanayokwenda wao.-

Baada ya Lucas kuwaeleza hivyo maaskari hao wa upelelezi, Gabriel na Saidi walimuuliza Lucas kuwa je baada ya mke wake kumueleza hivyo alifanyaje?

Lucas aliwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa bila hata ya kuuliza zaidi alimwambia mke wake Nancy kuwa sawa hamna shida amwambie tu huyo mtu aingie kwenye gari. Hivyo mke wake Nancy alimuita mtu huyo na kumwambia kuwa aje tu wampe lift.

Baada ya Lucas kuwajibu hivyo maaskari hao wa upelelezi walimuuliza Lucas na kumwambia kuwa je baada ya yeye kumruhusu mtu huyo kupanda kwenye gari yake na huyo mtu alivyopanda kwenye gari hilo kilitokea nini?

Baada ya maaskari upelelezi Saidi na Gabriel kumuuliza Lucas kuwa je baada ya yeye kumruhusu mtu huyo waliyekuwa wamempa lifti kupanda kwenye gari yake na huyo mtu alivyopanda kwenye gari hilo kilitokea nini? Lucas aliwajibu na kuwaambia maaskari hao kuwa anachokumbuka yeye ni kuwa huyo mtu alipanda kwenye gari lake na kukaa kwenye siti ya nyuma upande wake yeye Lucas na yeye akaondoa gari kuanza safari yao ya kurudi nyumbani kwao.

Baada ya Lucas kuwajibu hivyo maaskari hao walimwambia Lucas kuwa dunia kwasasa imeharibika sana na watu wamegeuka kuwa kama wanyama kiasi kwamba siku hizi watu hawaaminiani kirahisi kabisa sasa ni kitu gani hasa kilichomfanya yeye amuamini huyo mtu kwa haraka kiasi hicho na kumruhusu kupanda kwenye gari lake huku yeye akiwa hana wasiwasi wowote?

Lucas aliwajibu hao maaskari kuwa sababu kubwa ya kwanza iliyomfanya yeye asiwe na shaka wala wasiwasi wowote kuhusu mtu huyo ni kuwa kwanza alimkuta akiwa amesimama nje ya ofisi anazofanyia kazi mke wake na wakati anafika mahali hapo aliona huyo mtu na mke wake Nancy wakiwa wamesimama pamoja huku wakiongea hivyo bila ya kuwa na shaka wala wasiwasi wowote alijua kuwa labda huyo mtu atakuwa anajuana na mke wake na pia labda ni mfanyakazi mwenzake na ndio maana alimkubalia haraka haraka kumpa hiyo lifti, na sababu ya pili ya kumkubalia haraka haraka huyo mtu kumpa lifti ni kuwa huyo mtu wala alikuwa hatishi kabisa na alikuwa wa kawaida sana kwani hakuwa mtanashati sana na wala hakuwa akitisha au kuonekana muonekano wa kumtilia shaka kuwa ni jambazi au ni mwizi.

Baada ya Lucas kuwaambia hivyo maaskari hao, maaskari hao walimwambia Lucas kuwa kuna msemo wa lugha ya wenzetu ya kiingereza unaosema kuwa ?Dont? judge a book by its cover? ambao kwa lugha yetu ya Kiswahili unaweza kusema usimchukulie mtu au kitu kwa muonekano wake, hivyo siku nyingine asifanye maamuzi kwa kuangalia tu muonekano wa mtu bali atumie vigezo vingine. Na pia siku nyingine mtu akiombewa lifti hata kama baba yake mzazi yeye Lucas ndio anamuombea lifti mtu huyo inabidi amuulize kwanza huyo anayemuombea je anamfahamu huyo mtu anayetaka wampe lifti? Ili kama hamfahamu asimpe hiyo lifti na kama huyo mtu anamfahamu ndio ampe hiyo lifti.

Baada ya maaskari hao wa upelelezi kumwambia hivyo Lucas, Lucas aliwajibu sawa amewaelewa na hatakuja kufanya kosa hilo tena.

Maaskari hao waliendelea kumuuliza Lucas maswali mengine na hivyo walimuuliza tena kuwa tangu apatwe na matatizo hayo ya kuvamiwa na kupigwa risasi na huyo mtu ambaye walimsaidia kumpa lifti mpaka kupelekea yeye kulazwa hospitali na sasa ametoka hospitali na ana nafuu kidogo mpaka anaweza kuzungumza je amewahi kumuuliza mke wake Nancy kuwa yule mtu alikuwa ni nani? maana alimkuta akiongea naye yeye na ndio maana akamuamini na kuamua kumpa lifti. Lucas aliwajibu maaskari hao wa upelelezi na kuwaambia kuwa kwasababu ndio kwanza ametoka hospitali siku hiyo na yeye bado hajachangamka vizuri kusema ukweli hajakaa na kumuuliza mke wake kuhusu swali hilo ingawa hata yeye kwasasa ana shauku sana ya kufahamu kuhusu hilo.

Maaskari hao wa upelelezi waliendelea kumuhoji Lucas na walimwambia Lucas kuwa hebu aendelee kuwaelezea kuwa je safari yao ilikuwaje baada ya wao kuondoka hapo ofisini kwa mke wake Nancy.

Lucas aliwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa baada ya yeye na mke wake Nancy pamoja na huyo mtu waliyekuwa wamempa lifti kuondoka maeneo ya ofisini kwa mke wake wakiwa wameshakwenda mwendo wa dakika kadhaa yeye aliamua kumuuliza mtu huyo kuwa je yeye anaelekea wapi?

Baada ya Lucas kusema hivyo, hao maaskari walimuuliza Lucas na kumwambia kuwa huyo mtu alimjibu nini baada ya yeye kumuuliza swali hilo? Lucas aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa huyo mtu alimjibu na kumtajia sehemu anayoelekea ambayo ndio ilikuwa njia wanayoipita wao kwenda nyumbani kwao hivyo yeye Lucas alinyamaza na kuendelea kuendesha gari lakini ghafla alishangaa kuona anapigwa loba huku sauti kutoka nyuma ikimwambia kuwa atulie hivyo hivyo na aendelee kuendesha gari kwa utulivu huku akifata maelekezo anayopewa kwani akileta tu ukaidi atamuulia mbali hapo hapo.

Maaskari upelelezi Saidi na Gabriel walimuuliza Lucas na kumwambia kuwa je aliyesema hayo maneno alikuwa ni nani? Lucas aliwajibu maaskari hao wa upelelezi na kuwaambia kuwa aliyesema hayo maneno hakuwa mwingine bali alikuwa ni huyo huyo mtu waliyekuwa wamempa lifti. Baada ya Lucas kuwajibu hivyo hao maaskari wa upelelezi Saidi na Gabriel, maaskari hao walimuuliza tena Lucas kuwa wakati hayo yakiendelea mke wake Nancy yeye alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini? Lucas aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa huyo mtu alimwambia na mke wake huyo kuwa naye atulie na asifanye vurugu yoyote kwani akikiuka tu amri yake atamfumua ubongo wake na baada ya kusema hivyo alichomoa bastola. Lucas aliendelea kuwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa hivyo kama wanavyojua tena jinsi wanawake walivyo dhaifu na waoga hivyo hata mke wake Nancy baada ya kuambiwa tu hivyo alibaki tu akitetemeka na alishindwa kufanya chochote.

Baada ya Lucas kusema hivyo hao wapelelezi walimwambia Lucas kuwa asiwadharau wanawake kwani kuna wengine ni wabaya na wakatili kweli kweli sio kama anavyofikiria na inawezekana hata huo uoga aliouonyesha mke wake ni geresha tu au ni kweli alikuwa akiogopa. Baada ya maaskari hao kusema hivyo Lucas akawaambia maaskari hao kuwa kwahiyo wanataka kusema kuwa inawezekana mke wake Nancy anaweza kuwa amehusika kwa kiasi kikubwa kwenye hilo tukio!?

Wale maaskari walimwambia Lucas kuwa wao hawajasema hivyo na ndio kwanza wapo kwenye hatua za mwanzo kabisa za uchunguzi wa kesi hiyo ila walichokuwa wakimaanisha ni kuwa dunia ya sasa hivi sio ya kumdharau mtu hata kama ni mwanamke kwani siku hizi kuna wanawake ambao ni hatari kweli kweli sio kama zamani ambapo kazi kubwa ya wanawake ilikuwa ni kupika na kupakua na kulea watoto tu. Baada ya maaskari hao wa upelelezi kumwamabia hivyo Lucas waliendelea kumuuliza Lucas maswali mengine ili angalau kupata mwanga wa tukio hilo hivyo walimuuliza tena Lucas kuwa je baada ya hapo kiliendelea nini?

Baada ya Lucas kuulizwa swali hilo na maaskari hao wa upelelezi, Lucas alijibu na kusema kuwa baada ya kupata vitisho hivyo kutoka kwa huyo mtu waliyekuwa wamempa lifti yeye na mke wake Nancy ambaye alikuwa amekaa mbele kwenye kiti cha abiria pembeni yake walibaki wamechanganyikiwa kabisa na wasijue cha kufanya -tena na baada ya dakika kadhaa kupita yeye Lucas aliamua aanze kujitetea ili angalau mtu huyo awaachie na hivyo alianza kumwambia huyo mtu kuwa anaomba sana asimdhuru kwani atampa chochote atakachokitaka kutoka kwake lakini kwa mshangao wake mtu huyo alimjibu na kumwambia kuwa yeye hataki kitu chochote kutoka kwake bali anaitaka roho yake tu basi, hivyo asifanye vurugu yoyote bali asikilize kila atakachomwambia na atii kwa utulivu na ndio hapo alipogundua kuwa huyo mtu alikuwa yuko serious na alikuwa hatanii kabisa na alikuwa akitaka tu kumuua na si kuchukua chochote kutoka kwake kwani humo kwenye gari alikuwa na shilingi milioni moja cash, na pia saa aliyovaa yeye hata mke wake zilikuwa ni za gharama sana na hata simu yeye alikuwa nazo mbili ambazo ni za gharama sana na mke wake pia naye alikuwa nazo 2 ambazo nazo zilikuwa ni za gharama sana na pia kama wanavyojua wanawake kuvaa urembo kwani mke wake alikuwa amevaa mkufu shingoni na bangili kadhaa mikononi ambazo nazo zilikuwa ni za gharama sana lakini huyo mtu wala hakujisumbua kabisa kuangalia hivyo vitu.

Baada ya Lucas kusema hivyo, maaskari upelelezi Saidi na Gabriel waliendelea kuandika kwa dakika kadhaa baadhi ya maelezo waliyoyaona ni ya muhimu huku wakiendelea kumrekodi Lucas. Pia Lucas aliwaeleza maaskari hao kuwa baada ya huyo mtu kuchomoa bastola na kumwambia kuwa atulie na aendeshe gari kwa utulivu huku akisikiliza na kutii maagizo yake, huyo mtu alianza kumwambia kuwa aende njia ambayo alikuwa akimuelekeza yeye. Hivyo yeye kwa haraka haraka aliwaza kuwa hapo asipotumia akili yake ya kuzaliwa huyo mtu angeweza kumuua kweli hivyo ndio akaamua kufungua vioo vya gari kwa haraka sana na huku akiendesha kwa mkono mmoja alipiga kelele kuomba msaada, hivyo huyo mtu ndio akaamua kumpiga yeye risasi ya kwenye bega lake la kulia huku akimwambia kuwa si anajifanya mkaidi, sasa badala ya kumuulia huko alikokuwa akimpeleka atamuulia pale pale.

Baada ya kuwaeleza hivyo maaskari hao wa upelelezi hao, maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je ni nini kilitokea baada ya hapo? Lucas anasema kuwa kwa kweli baada ya kupigwa risasi hakumbuki tena kilichoendelea kwani alichanganyikiwa na baada ya dakika kadhaa hakujielewa tena.

Hao maaskari walimwambia Lucas kuwa baada ya huyo mtu kumpiga yeye risasi kwa jinsi ya maelezo aliyoyaandikisha mke wake polisi ni kuwa yeye Lucas alishindwa kulidhibiti gari na hivyo likapoteza muelekeo na ingawa yule mtu aliyekuwa nyuma ya hilo gari alijaribu kutaka kulidhibiti na kuliendesha akiwa bado huko kwenye siti ya nyuma lakini alishindwa na matokeo yake gari hilo liliacha njia na kupinduka na bahati hilo gari halikuwa kwenye mwendo mkali sana na ndio maana yeye na mke wake Nancy walipata michubuko kidogo ila hamna anayejua huyo mtu waliyempa lifti aliumia kwa kiwango gani kwani kwa maelezo ya mashuhuda wa ajali yao hiyo walisema kuwa mara baada ya huyo mtu kutoka kwenye gari lao hilo lililokuwa limepinduka huku akisaidiwa na watu waliofika mahali hapo kuwaokoa kwa haraka haraka walimuona akiwa na michubuko kidogo lakini mtu huyo hakuzungumza chochote kwani mara baada ya kufanikiwa tu kutoka kwenye gari hilo mtu huyo alipanda kwenye pikipiki ambayo ilikuwa imefika maeneo hayo na baada ya kupanda kwenye pikipiki hiyo mtu aliyekuwa anaendesha pikipiki hiyo akaondoa hiyo pikipiki kwa mwendo wa kasi sana kitu ambacho kimewafanya wao kugundua kuwa- hiyo pikipiki itakuwa ilikuwa ikiwafatilia toka mwanzo aidha toka yeye alivyotoka ofisini kwake au toka alivyotoka kazini kwa mke wake baada ya kumchukua mke wake na huyo mtu.
Maaskari hao wa upelezi Saidi na Gabriel waliendelea kumuuliza Lucas ambaye kwasasa alikuwa ameshaanza kuchoka na maswali yao na hivyo alitaka kupumzika. Hivyo walimuuliza tena Lucas kuwa je anampenda mke wake Nancy? Na hakuna malalamiko au manung?uniko yoyote kwenye ndoa yao hiyo? Lucas alibaki kuwashangaa hao wapelelezi kwa maswali yao hayo na hivyo aliwajibu na kuwaambia kuwa tangu amuoe mke wake Nancy miaka mitatu iliyopita na kujaliwa kupata mtoto mmoja mwenye miaka miwili sasa yani wamekuwa wakiishi kwa amani na furaha kubwa sana na mke wake huyo na wanapendana sana yani kupita maelezo.

Baada ya Lucas kujibu hivyo maaskari hao wa upelelezi walimwambia Lucas kuwa wao wamemuuliza swali kama anampenda mke wake Nancy na sio kama wanapendana na mke wake Nancy hivyo asiusemee moyo wa mwenzie bali ajisemee yeye mwenyewe, na pia wamemuuliza kama hakuna malalamiko au manung?uniko ya aina yoyote kwenye ndoa yao hivyo alitakiwa ayajibu maswali yao hayo na si vinginevyo.

Baada ya maaskari hao wa upelelezi kumwambia hivyo Lucas, Lucas aliwajibu maaskari hao wa upelelezi na kuwaambia kuwa ndio anampenda sana tena sana mke wake huyo na hakuna malalamiko au manung?uniko ya aina yoyote kwenye ndoa yao hiyo na amekuwa akijitahidi kufanya kila awezalo kumfanya mke wake huyo ambaye ni tulizo la moyo wake awe na furaha siku zote na sasa hivi hapo alipo wiki kama mbili zilizopita alikuwa amemuagizia mke wake huyo gari lingine tena la gharama sana kutoka Japan kama zawadi yake ya kumtunza yeye na mtoto wao vizuri na ameshamueleza kuhusu ujio wa hilo gari mke wake huyo.

Maaskari hao wa upelelezi Saidi na Gabriel wala hawakujali sifa alizokuwa akizitoa Lucas kwa mke wake Nancy na badala yake kimoyomoyo kila mmoja alisema kuwa wao wapo kazini tu hivyo walimuuliza Lucas kuwa je hivi karibuni amewahi kugombana na mke wake Nancy kwa kitu chochote au hata kama ni ugomvi mdogo tu, Lucas aliwajibu kuwa hapana. Na pia maaskari hao wa upelelezi walimuuliza Lucas na kumwambia kuwa hebu awaelezee kuhusu tabia ya mke wake Nancy anavyomfahamu kwa undani tangu wakiwa marafiki mpaka walivyooana na kubarikiwa kupata mtoto.

Lucas alianza kuwaeleza maaskari hao wa upelelezi kuwa amemfahamu Nancy kwa muda mrefu sana tangu wakiwa shuleni sekondari na tangu wameanza urafiki wao yeye na mke wake Nancy mpaka kufikia hatua ya kuoana siku zote anachojua ni kuwa mke wake huyo ni mwanamke mpole sana, mnyenyekevu, ana upendo sana, mchapa kazi, muda mwingi anapenda kuwa nyumbani na kufanya kazi za nyumbani, pia sio mtu wa mambo mengi, sio muongeaji sana na wala sio mkimya sana, pia hana tamaa kabisa yani sio kama mabinti na wanawake wengine waliojazana mjini hapo yani yeye mapenzi ni upendo na sio pesa na hata hayo magari na vitu vingine vingi vya thamani anavyomnunulia sio kwamba eti mke wake huyo ameomba au anaomba amnunulie -bali yeye mwenyewe Lucas ndio amekuwa akimnunulia na kumpa kutoka moyoni mwake na hiyo ndio sababu kubwa sana iliyomfanya yeye ampende Nancy na kuamua kumuoa kwani alianzana urafiki na Nancy wakiwa shuleni na yeye Lucas akiwa hana kitu kabisa na wazazi wake wala hawakuwa na utajiri bali walikuwa na maisha tu ya kawaida hivyo baada ya wazazi wake yeye Lucas kufariki waliwaachia urithi yeye na kaka yake Thomas na yeye urithi wake ndio akaamua kuanzisha hizo biashara zake mpaka kufikia hapo alipofika na ndio maana anamthamini sana mke wake Nancy kwani amemvumilia kwa mengi tangu wakiwa hawana kitu mpaka sasa amekuwa ni mfanyabiashara mkubwa.

Baada ya Lucas kusema hivyo maaskari hao wa upelelezi walimuuliza Lucas na kumwambia kuwa hivi hadhani kuwa labda kuanza kwake kuwa maarufu wakati yeye ni kijana mdogo kunaweza kuwa tishio kwa wafanyabiashara wakubwa hapa nchini na hivyo hicho kinaweza hasa kuwa chanzo cha yeye kuwindwa na wafanyabiashara wenzake wanaoshindana naye kwenye biashara zao hizo? Lucas aliwajibu maaskari hao wa upelelezi na kuwaambia kuwa yeye hafahamu kuhusu hilo ila labda inaweza kuwa hivyo maana siku zote wanadamu hatupendani na kila mtu anataka awe ni mwenye mafanikio peke yake.

Baada ya Lucas kuwajibu hivyo maaskari hao wa upelelezi, maaskari hao walimuuliza Lucas kuwa je hana ugomvi wowote na mfanyabiashara yeyote? Labda ugomvi wa kibiashara au hata mambo madogo madogo tu kama vile ya kuchukuliana wafanyakazi n.k? Lucas aliwajibu maaskari hao kuwa hapana hana ugomvi wa aina yoyote na mtu wa aina yeyote achilia mbali wafanyabiashara wenzake.

Baada ya Lucas kuwajibu hivyo maaskari hao wa upelelezi, maaskari hao wa upelelezi walimwambia Lucas kuwa hebu basi awatajie ni mfanya biashara yupi ambaye anaona labda hayuko naye sawa yaani hawana mahusiano mazuri hata kama kwa kusikia tetesi tu au anamuona labda hapendi mafanikio yake au anachokifanya au wanaushindani wowote wa kibiashara na kwenye biashara zao? Lucas aliwajibu maaskari hao kuwa hapana hamna mfanyabiashara yeyote ambaye anahisi kuwa anamchukia au amesikia kuwa anamchukia au ambaye anamuonyesha au amewahi kumuonyesha waziwazi kuwa hapendi mafanikio yake au hampendi yeye mwenyewe na hivyo kumchukia
SEHEMU YA TATU 3

Comments