Sehem ya - 4
Kesho yake ilivyofika wazazi wake Nancy pamoja na Thomas kaka yake Lucas walifika nyumbani kwa Lucas asubuhi na mapema. Walivyofika nyumbani hapo walimkuta Lucas akiwa ni mwenye mawazo na huzuni sana na wote kwa pamoja walimuuliza Lucas kuwa kwani siku hiyo waliyovamiwa kilitokea nini mpaka imepelekea mke wake Nancy kushikiliwa na maaskari hao wa upelelezi? Lucas aliwaambia kila kitu kilichotokea siku hiyo na hivyo alimalizia kwa kusema kuwa inawezekana wameamua kumshikilia Nancy kwasababu yeye ndio alimuombea lifti huyo mtu aliyetaka kumdhuru yeye, pia hata yeye mwanzo alijua kuwa Nancy alikuwa anamfahamu huyo mtu au labda alikuwa anafanya naye kazi ndio maana yeye akakubali kumpa lifti huyo mtu bila ya kuwa na wasiwasi wowote, sasa haelewi baada ya kuhojiwa huko polisi mke wake huyo amewaambia nini polisi ndio maana wameamua kumshikilia.
Baada ya maongezi ya hapa na pale kwa dakika kadhaa kati ya Lucas, Thomas na wazazi wake Nancy, mwishowe walikubaliana kuwa wadogo zake Nancy yaani Julia na Anthony wakae hapo nyumbani kwa kina Lucas ili Julia awasaidie wasichana wa kazi kumlea mtoto wa Lucas na dada yake Nancy yaani Henry kipindi ambapo wanaangalia uwezekano wa kumtafutia dhamana Nancy na pia kuangalia uwezekano wa kuimaliza hiyo kesi. Pia Lucas, Thomas pamoja na wazazi wake Nancy waliamua kuwa Anthony mdogo wake Nancy wa kiume naye akae hapo ili awe anamsaidia shemeji yake huyo kumpa kampani na kumsaidia kwa vitu vingi ambavyo yeye mwenyewe alikuwa bado hawezi kuvifanya mpaka apate msaada wa mtu. Ingawa Lucas alikuwa na wafanyakazi wawili lakini waliona kuwa uwepo wa mashemeji zake nyumbani hapo kwa kiasi fulani ungesaidia sana na pia ungemsaidia Lucas kuchangamka katika hiki kipindi kigumu alichokuwa anapitia.
Lucas na kaka yake Thomas pamoja na familia ya Nancy walijitahidi kumuwekea dhamana Nancy ili angalau akasubirie kesi yake akiwa nyumbani lakini polisi walikataa katakata kumpa dhamana huku wakisema kuwa kwanza kesi yake ni ya jaribio la kutaka kuua na pia isitoshe bado iko kwenye hatua za mwanzo kabisa hivyo wakimwachia kwa dhamana kwasasa wanaweza kuharibu ushahidi wao wote hivyo bado wataendelea kumshikilia ili aisaide polisi mpaka pale polisi watakaporidhika na ushahidi wao walioupata ndio dhamana ya Nancy itawekwa wazi.
Huko polisi nako maaskari upelelezi Saidi na Gabriel walienda kumuona bosi wao askari wa upelelezi Jamal ili kumueleza jinsi upelelezi wao ulipofikia ingawa ndio kwanza walikuwa kwenye hatua ya mwanzo kabisa.
Walivyofika ofisini kwa bosi wao huyo walikaribishwa na walivyokaa kwenye viti bosi wao huyo alianza kuwauliza je wana jipya lipi la kumueleza maana zimepita siku kama mbili tu tangu awatume kwenda kuipeleleza kesi ya mfanyabiashara Lucas. Baada ya bosi wao Jamal kuwauliza hivyo, maaskari upelelezi saidi na Gabriel walimwambia bosi wao huyo kuwa angalau wameanza kupata mwanga kidogo wa kesi hiyo na kwasasa wanamshikilia mke wa mfanyabiashara huyo. Bosi wao Jamal aliwauliza maaskari upelelezi hao Saidi na Gabriel kuwa kwanini wameamua kumshikilia mke wa mfanyabiashara huyo kwasasa na si mtu mwingine?
Maaskari hao wa upelelezi Saidi na Gabriel walianza kumwambia bosi wao huyo kuwa sababu moja iliyofanya wao kuamua kumshikilia mke wa mfanyabiashara huyo ni kuwa kwanza mke wake huyo ndio aliyemuombea lifti huyo mtu kwa mume wake Lucas ingawa kwasasa anakataa kuwa eti yeye hamjui kabisa huyo mtu na anasema kuwa alimuombea tu lifti huyo mtu kwa mume wake kwasababu huyo mtu alimwambia kuwa naye alikuwa akielekea maeneo wanayokwenda wao hivyo anaomba lifti. Lakini sababu nyingine kubwa sana iliyowafanya wamshikilie mke wake huyo ni kuwa Lucas aliongea na mke wake kwenye simu ambapo mke wake huyo ndio alikuwa amempigia na kumueleza kuwa anaomba akamchukue kwasababu gari lake lilikuwa ni bovu na amemuita fundi na fundi huyo alivyokuja kuliangalia amekuta ubovu wake ni mkubwa kidogo hivyo lisingeweza kupona siku hiyo sasa wao wamefikiria na kuona kuwa mtu pekee aliyekuwa anajua kuwa siku ile Lucas anakwenda kumchukua mke wake Kazini ni yeye Nancy mwenyewe, maana walijaribu kumuuliza Lucas kama kuna mtu yeyote aliyekuwepo wakati yeye akiongea na mke wake siku hiyo na Lucas alisema kuwa alikuwa tu peke yake sasa swali walilojiuliza ni kuwa kama kweli Nancy mke wa Lucas hamfahamu huyo mtu na labda huyo mtu ametumwa na wafanyabiashara wenzake Lucas au mtu yeyote ili kummaliza Lucas je huyo mtu alijuaje kuwa siku hiyo Lucas alikuwa anakwenda kumchukua mke wake Nancy kazini kwake na ndio maana yeye akaamua kumtuma mtu kwenda kumsubiria Lucas huko kazini kwa mke wake? Yani hilo ndio swali ambalo mpaka sasa linawatatiza na wakipata tu jibu la hilo swali basi kesi hiyo itakuwa imekwisha.
Maaskari hao wa upelelezi Gabriel na Saidi waliendelea kumwambia bosi wao huyo kuwa hivyo basi wao pia itabidi waende ofisini huko kwa Lucas ili angalau kuangalia mazingira ya ofisi hiyo kama kuna uwezekano wowote wa kugundua kitu kilichosababisha mawasiliano ya Lucas na mke wake Nancy kuvuja na kuwafikia hao walengwa waliotaka kumuua Lucas kama mke wake Lucas yaani Nancy hausiki kupanga uvamizi ule ingawa kwasasa asilimia zote zinamuangukia yeye Nancy.
Baada ya maaskari upelelezi hao kusema hivyo, bosi wao Jamal alishusha pumzi kidogo na kusema kuwa kwa kiasi fulani anaanza kukubaliana na wao kidogo walivyoamua kumshikilia huyo mke wa mfanyabiashara Lucas kwani inawezekana kabisa huyo mwanamke anajua au anahusika na huo mchezo maana huyo mfanyabiashara ana mali hivyo ukute huyo mke wake alikuwa anataka hizo mali za mume wake na akaona njia rahisi ya kuzipata hizo mali ni kumuua na matokeo yake mpango wake ndio hivyo tena haukufanikiwa.
Baada ya bosi wao Jamal kusema hivyo, maaskari upelelezi Gabriel na Saidi walimwambia bosi wao huyo kuwa hata wao kitu cha kwanza walichofikiria ni hicho na ndio maana wameamua kwanza kumshikilia yeye huku wakiendelea na uchunguzi wao kwani huyo mtu hakumgusa kabisa wala kumdhuru huyo mke wa Lucas zaidi tu ya kumpa vitisho, na huyo mke wa Lucas kuonyesha hali ya kuogopa na pia huyo mtu hakuwa anataka kitu chochote na alisema kabisa kuwa anaitaka roho yake Lucas basi na si kitu kingine chochote.
Baada ya maelezo hayo bosi wao Jamal aliwaambia kuwa inabidi waendelee kumshikilia tu huyo mwanamke mpaka pale watakapopata ukweli na pia asipewe dhamana yoyote kwasasa. Pia askari upelelezi Jamal aliwauliza vijana wake hao kuwa je baada ya kumshikilia huyo mwanamke wana mipango gani mingine? Maaskari upelelezi Saidi na Gabriel walimueleza bosi wao huyo kuwa kwasasa wamepanga kuwa kesho waende wakamuhoji huyo fundi wa gereji aliyeliangalia gari la mke wa Lucas inawezekana naye ni sehemu ya mtandao wao na inawezekana hilo gari la mke wake Lucas wala halikuwa bovu labda walicheza tu mchezo na huyo fundi wa gereji, hivyo wakienda kumuona huyo ndio wataujua ukweli na wamepanga kwenda kumuona fundi huyo wa gereji kesho. Baada ya Gabriel na Saidi kumwambia hivyo bosi wao huyo, bosi wao huyo aliwaambia kuwa anakubaliana nao na pia waendelee kumweleza kila hatua za upelelezi wa kesi hiyo zinapofikia.
Baada ya kuondoka ofisini kwa bosi wao maaskari wa upelelezi Saidi na Gabriel walirudi majumbani kwao kupumzika. Kesho yake walikwenda kumuona fundi aliyetengeneza gari la Nancy huko gereji kwake kama walivyokuwa wamepanga. Saidi na Gabriel walifika huko gereji kwa maelezo waliyokuwa wamepewa na Nancy mwenyewe pamoja na Lucas.
Walivyofika huko gereji walimkuta fundi huyo wa gereji akiwa anaendelea na kazi zake za kila siku na walivyosalimiana na kujitambulisha fundi huyo aliwakaribisha kwenye ofisi yake ndogo ambayo ilikuwa hapo kwenye gereji hiyo na maaskari hao walikaa juu ya matairi kwani hakukuwa hata na viti vya kukalia kwani kote kulikuwa kumezagaa spea na vifaa vingine vibovu vya magari.
Baada ya kukaa maaskari hao wa upelelezi walianza kumuuliza fundi huyo kuwa je anawafahamu Lucas na mke wake Nancy na anawafahamu kivipi? Fundi huyo alijibu na kusema kuwa ndio anawafahamu Lucas na Nancy wote wawili kwani ni wateja wake sana na yeye siku zote ndio huwa anawatengenezeaga magari yao yakipata ubovu au tatizo la aina yoyote na hata wakitaka kufanya service magari yao huwa wanafanyia hapo kwenye gereji yake.
Baada ya fundi hiyo kujibu hivyo maaskari hao wa upelelezi walimuuliza tena fundi huyo kuwa, je anakumbuka siku ile aliyoitwa na mke wa Lucas kazini kwake je mke huyo wa Lucas alimuitia nini? Fundi huyo alijibu na kuwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa mke huyo wa Lucas alimpigia simu siku hiyo na kumwambia kuwa gari lake lina matatizo kwani amepata shida sana kufika kazini kwake hivyo anaomba sana aende kazini kwake akamuangalizie gari lake hilo kwani hata kufika nalo mpaka kazini amefika nalo kibahati bahati tu.
Baada ya fundi huyo kusema hivyo maaskari hao wa upelelezi walimwambia fundi huyo kuwa je baada ya mke huyo wa Lucas kumwambia hivyo yeye alifanyaje? Fundi huyo aliwajibu na kusema kuwa yeye alimchukua kijana wake mmoja na wakaondoka na gari lake kuelekea huko kazini kwa Nancy.
Baaada ya fundi huyo kusema hivyo maaskari hao wa upelelezi walimwambia fundi huyo kuwa sasa hakuona shida kuiacha ofisi yake na yeye kuondoka na kwenda huko kazini kwa Nancy wakati tayari hapo alikuwa na kazi nyingi za wateja wengine? Fundi huyo aliwaeleza maaskari hao kuwa Lucas na mke wake ni wateja wake wakubwa sana tena sana na hivyo anawaheshimu sana, na hata siku moja hatapenda kuwapoteza kwani ni wateja wake wa uhakika hivyo baada ya yeye kupigiwa simu na Nancy hakuona shida kwenda huko ofisini kwa Nancy kuliangalia gari lake hilo kwani isitoshe yeye sio mara yake ya kwanza kwenda kumtengenezea Nancy gari lake ofisini kwake na hata Lucas pia amekuwa akienda kumtengenezea gari ofisini kwake na wakati mwingine hata nyumbani kwao kama ikitokea limeharibikia maeneo ya huko. Fundi huyo aliendelea kuwaeleza maaskari hao wa upelelezi kuwa na pia hapo kwenye gereji yake ana mafundi watano tena wa kuaminika kabisa na hivyo yeye alivyoondoka na fundi mmoja kwenda naye huko kazini kwa Nancy hao wengine wanne walibaki na kazi iliendelea kama kawaida na hakuna kitu kilichoharibika kabisa. Baada ya fundi huyo kusema hivyo maaskari hao wa upelelezi waliandika kwenye vitabu vyao walivyokuwa navyo na waliendelea kumuuliza fundi huyo maswali mengine.
Baada ya maaskari hao wa upelelezi kuandika kwenye vitabu vyao walivyokuwa navyo, waliendelea kumuuliza fundi huyo maswali mengine, hivyo walimuuliza fundi huyo kuwa kwanini aliamua kumchukua kijana huyo na si kijana mwingine yeyote kati ya wale wanne waliokuwa wamebaki?
Fundi huyo aliwajibu maaskari hao na kuwaambia kuwa aliamua kumchukua siku hiyo kijana huyo kwasababu hao vijana wake wote watano yeye anawaona kuwa wana ujuzi sawa na hivyo zikitokea kazi za kwenda nje kuwafata wateja huwa anamchukua kijana yeyote ambaye anakuwa hayuko bize sana kwa muda huo, sasa siku ile alivyoitwa na Nancy mke wa Lucas kwenda kumtengenezea gari lake ambalo lilikuwa limekorofisha hao vijana wake wanne wote walikuwa na wateja wamewasimamia ambao walikuwa wakisubiri magari yao yamaliziwe ili waondoke na huyo kijana aliyekwenda naye yeye alikuwa anafanya kazi ambayo ilikuwa haina haraka na alivyomuuliza kama ana kazi ambayo kuna mteja atakuja kuchukua gari muda sio mrefu au baada ya masaa machache yeye alijibu kuwa hana kazi ya kuimaliza kwa haraka siku hiyo isipokuwa wateja wake karibia wote wamesema kuwa wataenda kuchukua magari yao kesho au kesho kutwa na mengine tayari alikuwa ameshayakamilisha na ndio maana yeye aliamua kumchukua yeye na sio hao wengine.
Baada ya fundi huyo kujibu hivyo, maaskari hao wa upelelezi walimuuliza tena fundi huyo kuwa je hilo gari la Nancy lilikuwa na ubovu gani? Fundi huyo aliwaeleza maaskari hao ubovu uliokuwa kwenye gari hilo la Nancy na baada ya kuwaeleza maaskari hao wa upelelezi ubovu huo uliokuwa kwenye gari la Nancy maaskari hao walimuuliza fundi huyo kuwa je baada ya kugundua ubovu huo kwenye gari hilo la Nancy na yeye kuamua kuondoka nalo ili aje kulitengenezea kwenye gereji yake hiyo je gari hilo lilichukua muda gani kupona? Baada ya kuulizwa swali hilo fundi huyo alisema kuwa gari hilo lilichukua siku moja tu kutengemaa na hivyo kesho yake lilikuwa tayari. Baada ya fundi huyo kujibu hivyo maaskari hao walimuuliza fundi huyo na kumwambia kuwa je baada ya kuwa tayari nani alikuja kulichukua gari hilo kutoka hapo gereji kwake? Fundi huyo alijibu na kusema kuwa baada ya gari hilo kutengemaa aliamua kumpigia simu Nancy ili kumueleza kuhusu hilo kwani alikuwa anataka kumsikia yeye mwenyewe kama atasema anakwenda kulichukua hapo gereji kwake yeye mwenyewe au ampelekee kazini au nyumbani kwake lakini alivyopokea simu Nancy alimueleza kuwa wako hospitali kwani wamepatwa na matatizo ya kuvamiwa na mtu ambaye wanahisi kuwa ni jambazi na huyo mtu alitaka kumuua mume wake Lucas na ingawa hakufanikiwa lakini aliishia kumpiga mume wake risasi ya begani. Fundi huyo aliendelea kuwaambia maaskari hao wa upelelezi kuwa baada ya Nancy kumueleza hivyo alimwambia kuwa kwa kuwa wao muda huo walikuwa hospitali basi alipeleke hilo gari lake nyumbani kwao.
Baada ya fundi huyo kumaliza kusema hivyo, maaskari hao wa upelelezi Saidi na Gabriel walimuuliza fundi huyo kuwa je amelipwa shilingi ngapi baada ya kutengeneza gari hilo na je amelipwa pesa taslimu au amelipwa kwa njia gani? Na pia nani aliyempatia hizo fedha? fundi huyo aliwajibu na kuwaambia maaskari hao kuwa malipo ya kazi hiyo ya kutengeneza gari hilo la Nancy mke wa Lucas yalikuwa ni shilingi elfu 70 na bado hajalipwa pesa hizo kwani magari yote ya Lucas yakitengenezwa huwa wanandika tu gharama zinazostahili kulipwa na mwisho wa mwezi ndio wanawapelekea gharama zao na kampuni yake Lucas huwa ndio inalipa baada ya wao kuwapelekea hizo bili.
Baada ya fundi huyo kusema hivyo maaskari hao walimwambia fundi huyo kuwa hebu awape hivyo vielelezo vya risiti ambayo wameandika baada ya kumtengenezea mke wa Lucas gari lake. Fundi huyo alinyanyuka na kutoa faili ambalo wamekuwa wakiweka kumbukumbuku zote za matengenezo ya magari ya Lucas na akatoa risiti hiyo na maaskari hao wa upelelezi waliingalia na walijiridhisha kuwa kweli ubovu aliousema fundi huyo ndio huo ulioandikwa humo kwenye hiyo risiti na pia pesa aliyowatajia ya matengenezo ndio iliyokuwa imeandikwa humo hivyo baada ya kujiridhisha walimrudishia fundi huyo hiyo risiti naye alivyoipokea aliirudisha kwenye faili wanazoweka kumbukumbu zote za matengenezo ya magari ya Lucas na akalirudisha hilo faili mahali pake lilipokuwa pamoja na mafaili ya watu wengine na baada ya kulirudisha faili hilo akarudi kukaa mahali alipokuwa amekaa tangu mwanzo.
Fundi huyo alivyorudi kukaa maaskari hao walimuuliza fundi huyo kuwa je ana uhakika kabisa gari hilo la Nancy lilikuwa bovu au awaambie ukweli kama labda huyo mke wake Lucas yaani Nancy alimwambia wadanganye kuhusu ubovu wa hilo gari ili tu yeye afanye mambo yake. Yule fundi aliwaambia hao maaskari kuwa kusema kweli yeye aliitwa na kuambiwa kuwa gari ni bovu na yeye alivyofika kazini kwa Nancy akiwa na kijana wake aliyekwenda naye -waliliangalia hilo gari na kugundua kuwa kweli lilikuwa ni bovu na ndio maana wakalichukua kulitengeneza na si mambo mengine. Kwanza huyo dada mke wa Lucas alivyo mstaarabu na anavyojiheshimu na anajua kabisa kuwa yeye fundi yupo karibu sana na mume wake Lucas na pia yeye amemjua huyo Nancy kwasababu ya Lucas hivyo Nancy asingeweza kabisa kumwambia adanganye kuhusu hilo. Baada ya maelezo hayo ya huyo fundi wa gereji maaskari hao wa upelelezi Saidi na Gabriel walimwambia fundi huyo kuwa yeye akiwa kama fundi na mtaalamu hasa wa magari maana ingawa jina lake ni Ramadhani lakini wanasikia kuwa kwa utaalamu wake mpaka anaitwa Rama magari na hata gereji yake ndio inavyoitwa hivyo je wakati analitengeneza hilo gari la Nancy hakugundua chochote kama vile kuchokonolewa kwa vifaa vya gari hilo ili labda kulisababishia ubovu huo.
Fundi huyo huku akitabasamu alisema kuwa hapana hakugundua kitu chochote cha namna hiyo na hilo gari lilikuwa ni la kawaida tu kama lilivyo siku zote na hata kama kuna mtu alilichokonoa kwa makusudi ili lionekane bovu basi huyo mtu atakuwa na utaalamu wa hali ya juu sana kwani kwa kweli yeye na utaalamu wake wote aliokuwa nao hakugundua wala kuhisi kitu cha namna hiyo. Baada ya fundi huyo kujibu hivyo maaskari hao wa upelelezi walimshukuru sana kwa ushirikiano wake na walimwambia kuwa siku yoyote wanaweza kuja kumuona tena pale watakapohitaji maelezo yake mengine lakini kabla hawajaondoka wangependa kuongea na huyo kijana ambaye alikwenda naye kazini kwa Nancy kwa ajili ya kumtengenezea Nancy gari lake.
Baada ya maaskari upelelezi Saidi na Gabriel kumueleza fundi aliyemtengenezea Nancy gari lake kuwa kabla hawajaondoka wangependa kuongea na huyo kijana ambaye alikwenda naye kazini kwa Nancy kwa ajili ya kumtengenezea Nancy gari lake, fundi huyo aliwajibu maaskari hao kuwa hamna shida na hivyo alimuita huyo kijana na yeye alikwenda nje kuendelea na shughuli zake alizokuwa akifanya kabla maaskari upelelezi hao hawajafika hapo kwenye gereji yake.
Huyo kijana naye alivyofika maaskari hao walimwambia awaeleze kila kitu kilichotokea siku ile walivyofika ofisini kwa Nancy kwenda kulitengeneza gari lake ambalo lilikuwa bovu na kijana huyo aliwaeleza kila kitu na maelezo yake aliyoyaeleza hayakutofautiana kabisa na maelezo aliyoyatoa bosi wake fundi Rama magari, hivyo baada ya kumsikiliza kijana huyo maaskari upelelezi hao walimshukuru na wakaagana naye huku wakimwambia kuwa kama watahitaji kumuhoji tena watamtafuta.
Baada ya kumaliza kuwahoji mafundi hao waliotengeneza gari la Nancy, maaskari hao wa upelelezi waliondoka na kurudi ofisini ili kwenda kujadiliana walichoona baada ya kuwahoji mafundi hao. Na pia maaskari hao wa upelelezi waliona kuwa kwa maelezo waliyoyatoa mafundi hao hakukuwa na ulazima wowote wa kuwashikilia nao wa kwasasa ili kuisaidia polisi.
Walivyofika ofisini kwao maaskari upelelezi Gabriel na Saidi waliamua wachukue simu za Lucas na mke wake Nancy walizozitumia kuwasiliana siku hiyo waliyompa lifti huyo mtu aliyetaka kumuua Lucas ili kuangalia kama kuna mchezo wowote wa teknolojia uliofanyika kufatilia mawasiliano yao kwani kwa jinsi simu za siku hizi zilivyo inawezekana waliwekewa vitu kwenye simu zao bila ya wao kujua na hivyo mawasiliano yao yakawa yanafatiliwa.
Pia maaskari hao wa upelelezi waliamua kuwa itabidi kwenda huko kwenye makampuni ya simu kwenye mitandao waliyokuwa wakitumia mke wa Lucas, na fundi wa gereji ili wakajiridhishe kuwa Nancy mke wa Lucas na fundi wa gereji hawakuwa wakiwasiliana kuhusu mambo mengine yoyote zaidi tu ya kuwasiliana kuhusu ubovu wa gari la Nancy siku hiyo.
SEHEMU YA TANO 5
Comments
Post a Comment